JAMII YAASWA KUWA MAKINI INAPOWEKA TAARIFA BINAFSI MTANDAONI
Awareness 27 August 2026 3 min read

JAMII YAASWA KUWA MAKINI INAPOWEKA TAARIFA BINAFSI MTANDAONI

Jamii yashauriwa kuzingatia ulinzi wa Taarifa zao Binafsi pindi wanapotaka kuziweka kwenye Mitandao ya Kijamii.
Akizungumza katika mahojiano maalumu kupitia kipindi cha Kumepambazuka kilichorushwa hewani na Redio one leo Agosti 27, 2026, Afisa Habari Mwandamizi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) Bi. Joseline Chambasi ametoa wito kwa wananchi kuwa makini na Taarifa Binafsi wanazoziweka kwenye mitandao ya kijamii.
“Wito ninaotoa kwa watanzania ni kuhakikisha wanalinda Taarifa zao Binafsi kwakua zikitumika vibaya zinaweza kuleta madhara kwao au hata kwa familia zao. Hivyo kikubwa, kama si lazima usiweke Taarifa zako binafsi kwenye mitandao ya kijamii kwasababu hujui nani atakutana nazo na atazitumiaje.” Amesema Bi. Chambasi
Aidha Bi. Chambasi aliendelea kuwataka wananchi kutokuogopa kutoa Taarifa zao ili kupata huduma kwenye taasisi au ofisi mbalimbali nchini, bali wahakikishe wanatoa Taarifa zao na kupatiwa huduma kwenye Taasisi iliyosajiliwa na kupata vyeti husika kutoka PDPC.
“Mtu asiogope kupata huduma kwenye Taasisi yoyote bali ahakikishe amejiridhisha kuwa Taasisi hiyo imesajiliwa na ina vyeti halali kutoka PDPC” alisema Bi. Chambasi
Katika hatua nyingine Bi. Chambasi alitamatisha mahojiano hayo kwa kuzijulisha Taasisi na Ofisi zote nchini kwamba Kujisajili PDPC sio hiyari bali ni takwa la kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44 (PDPA).