Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imeanza mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wake wapya, ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uelewa na uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji, na hivyo kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Akifungua rasmi mafunzo hayo leo Oktoba 2, 2026 mkoani Tabora, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Mkilia, amesisitiza kuwa nafasi ya Utumishi wa Umma ni dhamana inayohitaji uadilifu, uwajibikaji, nidhamu, weledi na uzalendo.
“Kila taarifa mnayoifikia kupitia utekelezaji wa majukumu yenu ni dhamana inayopaswa kulindwa na kutumiwa kwa madhumuni halali” amesema Dkt. Mkilia, Mkurugenzi Mkuu, PDPC
Dkt. Mkilia amesisitiza umuhimu wa watumishi wa Tume kuzingatia usiri na uadilifu katika kushughulikia taarifa binafsi na faragha za wananchi, sambamba na kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Maadili ya Utumishi wa Umma.
Mafunzo hayo ya siku nne, kuanzia Oktoba 2 hadi 5, 2026, yanafanyika katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Ndaki ya Tabora, yakilenga kuwajengea watumishi wapya uelewa kuhusu Utumishi wa Umma, majukumu ya Tume, taratibu za kazi na maadili ya Utumishi wa Umma, ili kuwaandaa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa wananchi.