Watumishi wapya wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) wameendelea kujengewa uwezo kuhusu maadili, uadilifu na utoaji wa huduma bora kwa wananchi, ikiwa ni siku ya pili ya mafunzo elekezi ya awali yanayoendelea katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Ndaki ya Tabora.
Akiwasilisha mada kuhusu Misingi ya Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma, Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Ndaki ya Tabora, Bi. Lilian Shao, amesisitiza umuhimu wa watumishi kutekeleza wajibu wao kwa uaminifu wakati wote.
“Mtumishi anapaswa kutimiza wajibu wake kwa uaminifu hata kama hakuna mtu mwingine anayemuona.” Amesisitiza Bi. Lilian Shao.
Kwa upande wake, Meneja Mafunzo wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Ndaki ya Tabora, Bw. Richard Manase, akiwasilisha mada kuhusu Misingi Madhubuti ya Utoaji wa Huduma Bora kwa Wateja, amewataka watumishi kuwahudumia wateja wa taasisi kwa namna ambayo wao wenyewe wangependa kuhudumiwa.
Katika mada kuhusu Athari za Rushwa katika Utumishi wa Umma, Bw. Manase ameeleza kuwa rushwa katika Utumishi wa Umma ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka ya umma kwa manufaa binafsi, kupindisha sheria na kufanya upendeleo, na kusisitiza umuhimu wa watumishi kuzingatia uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mada hizo zinawaandaa watumishi wapya kutambua kuwa huduma bora kwa wananchi inaanzia kwa mtumishi mwadilifu, anayewajibika, anayezingatia sheria na maadili na anayemthamini mwananchi anayemhudumia.
Mafunzo hayo ya siku nne yanalenga kuwajengea watumishi wapya maarifa, maadili na mtazamo wa kiutumishi utakaowawezesha kutekeleza majukumu ya PDPC kwa weledi, uwajibikaji na kutoa huduma bora kwa wananchi.