UZINGATIAJI WA SHERIA NA TARATIBU WASISITIZWA KATIKA UTENDAJI WA WATUMISHI
Event 4 October 2026 3 min read

UZINGATIAJI WA SHERIA NA TARATIBU WASISITIZWA KATIKA UTENDAJI WA WATUMISHI

Watumishi wapya wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) wameendelea kuimarishiwa uelewa kuhusu sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza utendaji na uendeshaji wa shughuli katika ofisi za umma, ikiwa ni siku ya tatu ya Mafunzo Elekezi ya Awali yanayoendelea katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Ndaki ya Tabora.

Akiwasilisha mada kuhusu Menejimenti ya Kumbukumbu na Uendeshaji wa Ofisi, Mkufunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Ndaki ya Tabora, Bw. Musa Migabo, amewajengea watumishi uelewa kuhusu dhana na misingi ya utunzaji na usimamizi wa kumbukumbu katika ofisi za umma.
Bw. Migabo ameeleza kuwa Kifungu cha 9 cha Sheria ya Kumbukumbu na Nyaraka ya mwaka 2002 kinaweka wajibu kwa wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kuhakikisha kumbukumbu zinazohusu kazi na shughuli za ofisi zinazalishwa na kutunzwa ipasavyo.
Kwa upande wake, Mkufunzi wa Chuo hicho, Bw. Brevius Rudovick, amewawezesha watumishi kupitia mada kuhusu Mapitio ya Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, pamoja na Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022 na Kanuni za Kudumu za mwaka 2009.
Katika mafunzo hayo, Bw. Rudovick amesisitiza kuwa shughuli zinazotekelezwa na watumishi katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na maamuzi wanayofikia lazima yawe ndani ya matakwa ya Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake, ikiwa ni msingi wa kuhakikisha utendaji unaozingatia sheria, taratibu na uwajibikaji.
Mafunzo hayo yanaendelea kuwajengea watumishi wapya msingi wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na kuzingatia mifumo ya kisheria na kiutendaji, na hivyo kuchangia katika ufanisi wa Tume na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.