Watumishi wapya wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) wamehitimisha Mafunzo Elekezi ya Awali yaliyolenga kuwajengea maarifa, uelewa na misingi ya kiutumishi itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu, uwajibikaji na kuzingatia sheria na taratibu.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Ndaki ya Tabora, Bw. Dastan Kingalu, amewapongeza washiriki kwa kushiriki mafunzo hayo na kueleza imani yake kuwa maarifa waliyoyapata yatawawezesha kuwa watendaji wazuri katika utekelezaji wa majukumu yao.
Bw. Kingalu amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kina jukumu la kuwajengea uwezo watumishi wa umma katika hatua mbalimbali za maisha yao ya kiutumishi, kuanzia wanapoajiriwa, wanapokuwa kazini hadi wanapokaribia kustaafu, ili kuimarisha utendaji na utoaji wa huduma katika Utumishi wa Umma.
Katika kipindi cha siku nne za mafunzo, watumishi hao wamejengewa uelewa katika maeneo mbalimbali yakiwemo majukumu ya msingi ya PDPC na utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi; maadili na utendaji katika Utumishi wa Umma; utoaji wa huduma bora; athari za rushwa; menejimenti ya kumbukumbu na uendeshaji wa ofisi; pamoja na sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza Utumishi wa Umma.
Mafunzo hayo yamehitimishwa kwa washiriki kutunukiwa vyeti vya kutambua ushiriki wao, ikiwa ni hatua ya kuhitimisha mafunzo yaliyowaandaa kuwa na msingi imara wa kutekeleza majukumu yao na kuchangia katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.