KONGAMANO LA KWANZA LA FARAGHA NA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI TANZANIA LAFUNGULIWA RASMI
Event 29 June 2026 3 min read

KONGAMANO LA KWANZA LA FARAGHA NA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI TANZANIA LAFUNGULIWA RASMI

Kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Angella Jasmine Mbellwa Kairuki (Mb), leo Juni 29, 2026 Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb) amefungua rasmi Kongamano la Kwanza la Kitaifa la Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi la mwaka 2026.
Akifungua kongamano hilo, Mhe. Mkama amesema kuwa uchumi wa kidigitali tunaoutamani hauwezi kujengwa juu ya teknolojia pekee bali unahitaji kuaminiana kati ya wananchi, Serikali, taasisi za umma na sekta binafsi kupitia mfumo madhubuti wa ulinzi wa taarifa binafsi.
“Ni vyema kuwa na kongamano rasmi la masuala ya faragha na ulinzi wa taarifa binafsi kwa lengo la kukutana kwa pamoja na kujadiliana maswala muhimu yanayohusu faragha na ulinzi wa taarifa binafsi na kuwa na mwelekeo wa pamoja kama taifa” amesema Mhe. Mkama.
“Kwa sasa huduma nyingi za Serikali na taasisi binafsi zinatolewa kupitia mifumo ya TEHAMA na kumekuwa na jitihada za kuhakikisha mifumo hiyo inasomana na kubadilishana taarifa. Ni vyema mifumo hiyo inapobadilishana taarifa izingatie misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi inayokubalika kitaifa, kikanda na kimataifa na hivyo imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi itaongezeka” amesema Mhe. Mkama
Mhe. Mkama pia ameipongeza kwa dhati bodi na menejimenti ya PDPC kwa kuandaa kongamano hilo na kusema kuwa kongamano hilo limekusudia kuifanya Tanzania kuwa jukwaa la kitaifa na kikanda la kubadilishana uzoefu, kujifunza na kujenga ushirikiano wa faragha na ulinzi wa taarifa binafsi.
PDPC ni taasisi muhimu ya kujenga imani ya wananchi katika Uchumi wa kidigitali kwa kuhakikisha uzingatiaji wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa taasisi za umma na binafsi unaonwa kama sehemu ya kujenga Imani ya wananchi kwao kwa kuhakikisha zinawekeza katika mifumo salama ya usimamizi wa taarifa na kujenga uwezo wa watumishi wao.
Kongamano hilo la Kwanza la Kitaifa la Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi la mwaka 2026 lenye kauli mbiu isemayo faragha kama nguzo, ulinzi wa kidigitali jumuishi kuelekea dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2050 litafanyika kwa siku tatu kuanzia leo tarehe 29 Juni, 2026 katika ukumbu wa mikutano wa Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na limehudhuriwa na washiriki zaidi ya 800 kutoka ndani na nje ya Tanzania.