Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) na Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) leo Jumatatu tarehe 13, Julai 2026 wamezindua rasmi Programu ya Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi Waliothibitishwa (Certified Data Protection Officers Program).
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC amesema licha ya taasisi nyingi kutekeleza takwa la kuteua Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi, imebainika kuwa maafisa hao wana taaluma na viwango tofauti vya uelewa wa dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi.
"Ushirikiano wa PDPC na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni msingi imara wa kujenga wataalamu wenye weledi wa kweli katika fani ya ulinzi wa taarifa binafsi. Mafunzo haya yapo kisheria na ni lazima kwa kila DPO aliyeteuliwa kuyapata ili kuhakikisha anatekeleza Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kikamilifu," amesema Dkt. Mkilia.
"Nitoe rai kwa viongozi wa taasisi zote kuwawezesha DPOs wenu kushiriki programu hii. Hii ndiyo njia ya kuimarisha utawala bora na kujenga imani ya wananchi katika huduma mnazozitoa," amesisitiza Dkt. Mkilia.
Wakati huo huo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Alex Makulilo, amesema kuwa programu hii si semina ya kawaida, bali ni mafunzo mahususi na ya kina yatakayofundishwa kwa nadharia na vitendo.
“Uteuzi pekee wa Afisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi hauwezi kutosha kusimamia utekelezaji wa sheria. Ndiyo maana PDPC imekichagua Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kutoa mafunzo hayo bila kuathiri utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ya Maafisa hao katika vituo vyao vya kazi. Washiriki watakuwa huru kusoma kozi hii kwa njia tofauti tofauti” amesema Profesa Makulilo.
“Mafunzo haya yatatolewa kwa awamu, awamu ya kwanza ya Programu hii itaanza rasmi tarehe 10 Agosti, 2026 na itakuwa na moduli tano, itafundishwa kwa muda wa siku 14 na itagharimu Tsh. 2,500,000 kwa kila mshiriki na mwisho wa mafunzo hayo, washiriki watafanyiwa tathmini ya kina na kisha kuthibitishwa na PDPC” amesema Profesa Makulilo.
Dhamira kuu ya Tume ni kuona Tanzania inakuwa na Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi wenye ujuzi, weledi na umahiri mkubwa wa kutekeleza majukumu yao kwa kufuata kikamilifu matakwa ya sheria ya kulinda faragha za watu.