TUME ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), imewataka watumishi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Zanzibar kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, ikiwemo kuhakikisha wanapata ridhaa ya wahusika taarifa wakiwemo wanafunzi kabla ya kutumia taarifa hizo.
Afisa Rasilimali watu wa PDPC Ofisi ya Zanzibar, Bw. Amour Ali Abdallah ameyasema hayo wakati akitoa mafunzo ya uelewa kuhusu dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa wafanyakazi wa bodi hiyo, ofisini kwao Kwamchina Zanzibar.
“Taarifa zinazokusanywa na kuchakatwa wakati wa usajili wa wanafunzi, zikiwemo namba za NIDA au Mzanzibari Mkaazi, majina, anwani za makazi na taarifa za elimu hizo ni taarifa binafsi zinazopaswa kulindwa dhidi ya matumizi yasiyokusudiwa na ni lazima kupata ridhaa ya wahusika pale inapohitajika” amesema Bw. Amour Ali Abdallah.
Afisa huyo alibainisha kuwa kabla ya kupiga picha au kutumia majina ya washiriki katika machapisho, mitandao ya kijamii na majukwaa mengine ya mawasiliano, ni muhimu kuwajulisha wahusika na kupata ridhaa zao ikiwa ni sehemu ya kuheshimu haki zao za faragha.
Alifafanua kuwa hata pale mtu anapokuwa amesaini fomu ya kuruhusu matumizi ya taarifa zake, endapo atabadilisha uamuzi na kueleza kutotaka picha au taarifa zake zichapishwe, taasisi inapaswa kuheshimu matakwa yake kwa kuzingatia sheria.
Alitoa mfano wa nyaraka za wanafunzi na mikataba inayoweza kuachwa katika maeneo yasiyo salama, kwani hali hiyo inaweza kusababisha taarifa muhimu za wahusika kufikiwa na watu wasiokuwa na mamlaka ya kuziona.
Alibainisha kuwa jukumu la kulinda taarifa binafsi halipaswi kuishia kwa viongozi wa taasisi pekee, bali linapaswa kuzingatiwa na wafanyakazi wote, wakiwemo watumishi wa masjala, rasilimali watu na viongozi wengine.