WATUMISHI PDPC WAPEWA ELIMU YA LISHE NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA
Awareness 30 April 2026 3 min read

WATUMISHI PDPC WAPEWA ELIMU YA LISHE NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

'Ni muhimu kufuata kanuni za ulaji ulio bora ili kuepuka uzito uliokithiri utakaosababisha kupata magonjwa yasiyoambukiza'

Watumishi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) leo Aprili, 30 wamepatiwa elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza pamoja na umuhimu wa kuzingatia lishe.

Wakitoa elimu hiyo, Dkt. Florence Malamso pamoja na Afisa Tabibu wa lishe Mussa Kasela wametahadharisha kuwa watumishi wapo katika hatari ya kupata magonjwa sugu yasiyoambukiza kutokana na mwenendo wa maisha usioridhisha ikiwa ni pamoja na kutokuwa na tabia ya kufanya mazoezi na ulaji usiozingatia mpangilio sahihi wa lishe.

“Kwa kawaida asilimia kubwa ya watumishi wakiwa ofisini wanafanya kazi zinazowalazimu kukaa muda mrefu, lakini pia wengi hawana utaratibu wa kufanya mazoezi hali inayopelekea wengi wao kupata magonjwa sugu yakiwemo kisukari, shinikizo la damu, figo na ugonjwa wa ini. Mnapokuwa kazini muwe na utaratibu wa kutenga muda wa kutembea tembea ili kuruhusu mzunguko mzuri wa damu mwilini” amesema Dkt. Florence Malamso.

“Ni muhimu kufuata kanuni za ulaji ulio bora ili kuepuka uzito uliokithiri utakaosababisha kupata magonjwa yasiyoambukiza. Pia watumishi wawezeshwe kushiriki katika michezo ili kuimarisha afya ya akili na mwili’ amesema Afisa tabibu Mussa Kasela.

Kwa upande wake Bi. Rehema Abdalla, Mkurugenzi wa Ofisi ya PDPC Zanzibar kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu PDPC Dkt. Emmanuel Mkilia, akiwakaribisha wawezeshaji hao aliwashukuru kwa kufika kutoa elimu hiyo muhimu ya afya na kuwahakikishia kuwa PDPC itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watumishi ili kuhakikisha usalama wa afya zao na kuimarisha utendaji wao wa kazi.